HANS POPPE MIKATABA YA SIMBA HUWA WAZI...SOMA HAPA ALICHOKISEMA KUHUSIANA NA MAAMUZI YAKE YA KUACHIA NGAZI
Zacharia Hans Poppe, mmoja wa wanachama na viongozi maarufu wa Klabu ya Simba, ameamua kuachia ngazi kwenye kamati ya utendaji.
Uamuzi wake wa kuondoka kamati ya utendaji, moja kwa moja unamuondoa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa kamati ya usajili.
Hans Poppe amesema kuwa, ameondoka baada ya jopo lililoongozwa na Rais wa Simba, Evans Aveva kuingia mkataba na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportsPesa ambao wamesaini mkataba wa Sh bilioni 4.9 kwa miaka mitano.
Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili, Hans Poppe amesisitiza, ameamua kukaa pembeni.
“Nitabaki kama mwanachama wa kawaida wa Simba. Nitaendelea na shughuli zangu nyingine,” alisema na alipoulizwa sababu za kujiuzulu alisema.
“Mambo yamekwenda kwa uficho, mkataba umekuwa ukifichwa. Kamati ya utendaji imetaarifiwa siku moja kabla ya kusainiwa. Ilikuwa Alhamisi, Ijumaa wamesaini, nini kinafichwa.
“Mimi nakaa pembeni, nimeshaandika na barua. Sitaki kuwa sehemu ya watu wasio waungwana. Angalia hata Mo Dewji hakuwa akijua, lakini huyu mtu mwaka mzima ndiye katukopesha mishahara.
“Dewji alisema, mkitaka kusaini mkataba kama mmepata mdhamini mniambie. Maana na yeye tulimpa jukumu la kutafuta mdhamini, hata mimi nilipewa jukumu hilo lakini leo unasikia wenzako wameingia mkataba na mdhamini mpya.
“Kabla tumekuwa tukishirikiana kwa kila jambo, kwenye shida na raha. Vipi leo, nini kimefanya tusiwe pamoja?
“Kawaida walitakiwa waje na mkataba, tuujadili na kuangalia vipengele. Kama kuna sehemu zikarekebishwe au kuongezwa vifanyiwe kazi, mwisho wakija tuseme hapa sawa, basi usainiwe. Nani atakataa mdhamini kama unaona ana faida na klabu?” alihoji Hans Poppe.
Hans Poppe ndiye amekuwa injini ya usajili katika usajili katika kikosi cha Simba.
Post a Comment