HII HAPA KAULI YA MBOWE BAADA YA SERIKALI KUHARIBU MIUNDO MBINU YA SHAMBA LAKE
Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe amethibitisha shamba lake kuvamiwa na viongozi wa serikali ya Wilaya na kuharibiwa miundombinu ya shamba hilo huku akidai anajua yote hayo yanafanyika kutokana na misimamo yake ya kisiasa na kudai hawawezi kumbadili.
Freeman Mbowe amesema hayo leo kupitia mitandao yake ya kijamii huku akikiri wazi kuwa siku ya Alhamisi ya tarehe 7 mwaka huu walipokea barua kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira -NEMC ambayo ilikuwa inadai kilimo wanachofanya kilikuwa kinaharibu mazingira hivyo hawapaswi kuendelea na kilimo hicho.
"Ni kweli nimepata taarifa ya kuwa mkuu wetu wa wilaya ya Hai, akiambatana na askari wa mgambo akiambatana na watu wengine ambao sijaweza kuwafahamu wakiwemo vile vile waandishi wa habari, walikwenda kwenye mradi wetu wa Kili Vegies ni mradi wa kilimo cha kisasa cha mboga mboga (Green house), tukilima mboga na matunda, tukilima mboga kwa sababu ya 'local market' na wakaanza kuharibu miundombinu, ikiwemo kuharibu 'Green houses', kukatakata mabomba , kuharibu mimea na uharibifu mwingine mwingi" alisema Mbowe n kuongeza;
"Ni kweli tulipokea barua ya NEMC siku ya Alhamisi tarehe 7, iliandikwa tarehe 7 lakini tuliipata tarehe 8, tulijibu hiyo hoja ya NEMC, kwamba tunaamini wamekosea sheria kwa sababu kilimo chetu hakiharibu mazingira wala shutuma zilizotolewa kwamba ni kwenye chanzo cha maji sio kweli, wanadai kwamba shamba hilo limeanzishwa kwenye chanzo cha mto Weruweru jambo ambalo sio kweli, mto unaoitwa Weruweru unaanzia mlimani kabisa National Park Kilimanjaro"
Mbowe anasema kitendo hicho kilichofanywa na viongozi hao ni kitendo cha kufedhehesha na cha kukatisha tamaa hivyo anasikitishwa sana na kitendo hicho, huku akisema anatambua kuwa yote hayo anayofanyiwa ni kutokana na misimamo yake kisiasa, na misimamo ya chama anachokiongoza.
"Najua haya yanatokea kwa sababu ya misimamo yangu ya kisiasa kwa sababu wa muelekeo wangu wa kisiasa na uthabiti na uimara wa chama ninachokiongoza, sasa mimi siwezi kuwa kondoo, nimesema siku zote, haya mambo ya duniani anayeyalipa ni Mungu,hawatabadilisha mawazo yangu kwa kuharibu mali zangu, wanaweza kuharibu zote hata wakitaka roho yangu waichukue, waichukue tu lakini haitanisababisha nibadili msimamo wangu katika kuamini ninachokisimamia, ninachokipigania katika Taifa" alisisitiza Mbowe
Mbali na hilo kiongozi huyo amedai kuwa hakuna wingi wa mali zake zinaweza kuharibiwa zikamfanya yeye akapige magoti kama watu wengine wanavyofanya, anadai yeye hawezi kupiga magoti bali atasimama kwenye ukweli na haki siku zote.
Hili ni tukio la pili kwa mwaka huu kutokea kwenye shamba hilo, mwezi wa kwanza mwaka huu serikali ilimtaka kiongozi huyo kusimamisha kilimo kwenye shamba hilo ikidai kuwa lipo kwenye chanzo cha maji.
Post a Comment