Mwigulu awataka waliosaini mikataba mibovu ya madini wajitokeze hadharani kueleza wanamaslahi gani na kampuni wanazo zitetea?
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ametaka wanasheria wakuu wa Serikali wastaafu waeleze hadharani maslahi waliyonayo kwenye kampuni za madini zinazosafirisha mchanga nje ya nchi.
Hatua hiyo ya waziri imekuja siku chache baada ya wanasheria wakuu wastaafu waliofanya kazi kwa nyakati tofauti wakati nchi ikiingia kwenye mikataba ya madini ‘kujivua lawama’ kuhusu udanganyifu uliogunduliwa kuhusa sakata la usafirishaji wa mchanga.
Wanasheria hao wakuu wa Serikali wastaafu ni Andrew Chenge na Jaji Frederick Werema na amewataka wamwache Rais Dk. Magufuli aendelee kulinda rasilimali za umma zisiliwe na watu wachache.
Mwigulu amesema hayo juzi, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Tarafa ya Ndago, Jimbo la Iramba.
Alisema Chenge na Werema kwa nyakati tofauti wakiwa wanasheria wakuu wa serikali, pamoja na majukumu yao mengine, wameshiriki kusaini mikataba mikubwa mikubwa, ikiwamo ya makampuni ya kuchimba madini.
“Kwa akili ya kawaida tu, baadhi ya mikataba mikubwa, ikiwamo ya makampuni ya madini, haikuwa sawa… ndiyo maana imelalamikiwa kwa muda mrefu.” alifafanua Mwigulu, Mbunge wa Jimbo la Iramba.
Alisema juzi juzi magazeti yameeleza kuwa akina Chenge na Werema wamedai kuwa Rais wetu Magufuli amedanganywa na tume maalumu ya Profesa Mruma.
“Wao ndio waliosaini mikataba ambayo imechangia Taifa kupoteza mabilioni ya fedha kupitia usafirishaji wa michanga nje ya nchi. Sasa wamegeuka na kuwa upande wa pili wa watu waliosaini pamoja mikataba hiyo mibovu. Nawashauri watoke hadharani…. waeleze wana maslahi gani na kampuni wanazozitetea,” alifafanua zaidi.
Aidha, Mwigulu amesema Chenge na Werema wakishindwa kuweka wazi maslahi waliyonayo, basi ni vema wakakaa kimya na kumwacha Rais wa vitendo aendelee kuinyoosha nchi.
“Hivi ukimpa mtu kazi ya kuuza duka, halafu kila siku awe anakuambia hajauza kitu na huku akilalamika kuwa kila siku anapata hasara. Unamshauri aachane na biashara inayompatia hasara, haachi…anaendelea kuwepo tu, utamwalewaje. Si atakuwa si mkweli, mwongo ananufaika na hilo duka,” alisema.
Akiijengea nguvu hoja yake, alisema Chenge na Werema wanaishi Masaki, jijini Dar es Salaam, hawa hawawezi au watakuwa wamesahau maisha ya Watanzania wengi maskini waliopo vijijini. Hivyo wamwache Rais Magufuli ambaye ameonyesha uzalendo wa kweli, aendelee kulinda rasilimali za umma.
Alisema kwa wao wanaomfahamu Rais Magufuli, kwa hili la kuchokonoa kwenye madini na kubaini upotevu mkubwa wa fedha za umma, ni mwanzo tu, kazi bado ipo mbele ya kuchokonoa zaidi ubadhirifu na wizi wa mali ya umma katika sehemu mbalimbali.
Mwigulu ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wazalendo wa madhehebu ya dini mbalimbali waendelee kumwomba Mungu ampe Rais Magufuli afya njema na ujasiri wa kuziba mwinya yote inayotia hasara Taifa letu.
Post a Comment