''YANGA WANA TIMU NZURI NA KINACHOTAKIWA NI KUJUA NINI WAFANYE NINA IMANI WANAFAHAMU ILI KUWEZA KUPATA MATOKEO MAZURI'' MSUVA.


Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simon Msuva, amewapa neno wachezaji wa kikosi hicho akisisitiza kuwa wana uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu lakini wakirekebisha vitu vidogo.


Msuva ambaye anaichezea Klabu ya Difaa Al Jadida ya nchini Morocco, aliichezea kwa kiwango timu hiyo ikiwa ni pamoja na kutwaa nafasi ya ufungaji bora akifungana na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting kwa kufunga mabao 14 kila mmoja.


Yanga ambayo ipo nafasi ya sita ya msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi tisa, imeonekana kuanza kwa kusuasua kwenye ligi ya msimu huu kufuatia kushinda michezo miwili na kutoa sare mitatu huku wapinzani wao Simba wakiongoza kutokana na kuwa na pointi 11 hadi sasa, sawa na Mtibwa Sugar, wakipishana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.


Msuva amesema kuwa, kiujumla timu hiyo ni nzuri lakini wanatakiwa kujitathimini kujua wapi kuna tatizo ili kuweza kutatua kuhakikisha wanafanikiwa kufanya vyema katika michezo yao inayofuata.


“Yanga wana timu nzuri na kinachotakiwa ni kujua nini wafanye lakini nina imani wanafahamu ili kuweza kupata matokeo mazuri wanatakiwa kufanya nini.


“Wachezaji wapo vizuri kikubwa wanachotakiwa kukiangalia ni kujiamini kama vile mwalimu anavyowaamini wao na wasiteteleke na matokeo ya Simba kwani nina matumaini makubwa kuwa watafanya vyema msimu huu.



“Kikubwa ni pointi tatu ili kuwapa mashabiki kile ambacho wanakihitaji mwisho wa siku kutetea ubingwa,” alisema Msuva.

No comments

Powered by Blogger.