Yanga wamevuliwa ubingwa wa FA Cup Mwanza
Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya soka la Tanzania Mbao FC ya mkoani Mwanza imefuzu kucheza fainali ya FA Cup au maarufu kama Azam Sports Federation Cup kwa kuwatoa mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga SC.
Wakiwa wamepanda daraja kutoka ligi kuu Tanzania bara kwa mara ya kwanza, wameweza kufuzu kucheza fainali ya kwanza katika historia yao kwa kuifunga Yanga kwa goli 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Goli pekee lililoipa ushindi Mbao FC lilitokana na kujifunga kwa beki wa kati wa Yanga Vicent Andrew dakika ya 27 kipindi cha kwanza wakati akiwa katika harakati za kuokoa krosi iliyopigwa na Pius Buswita wa Mbao FC.
Matokeo hayo yanaivua Yanga ubingwa wa FA Cup (Azam Sports Federation Cup) ubingwa ambao waliutwaa mwaka uliopita kwa kufunga Azam kwenye mchezo wa fainali.
Mbao watakutana na Simba kwenye mchezo wa fainali mechi ambayo Simba ndio wanatarajiwa kuwa wenyeji kwa sababu ndio walikuwa wa kwanza kufuzu kucheza fainali baada ya kuifunga Azam FC kwenye mchezo wa nusu fainali uliochezwa jana kwenye uwanja wa taifa.
Kwa upande wa Yanga, wanalazimika kutumia vyema michezo yao ya ligi kuu Tanzania bara kwa sababu ndio njia pekee ambayo itawafanya washiriki michuano ya kimataifa ikiwa watashinda ubingwa.
Post a Comment