HATIMAYE KAMUSOKO ARUDISHWA KIKOSI CHA TIMU YA TAIFA


Kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko ameitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe kinachojiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Liberia mwezi ujao.


Kocha Norman Mapeza ameamua kumuita Kamusoko kikosini kwa ajili ya mchezo wao wa kuwania kufuzu fainali za Afrika baada ya kutoitwa kwa muda mrefu katika timu hiyo.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuitwa kikosini, Kamusoko alisema anamshukuru Mungu baada ya kuchaguliwa kwenye kikosi hicho.


“Kweli nawashukuru sana watu wote wa Yanga hasa benchi lote la ufundi kwa namna walivyokuwa wakiniamini na kunipatia nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.


“Naamini chachu ya mimi kuitwa timu ya taifa inatokana na Yanga na ndiyo maana leo utaona nimeitwa kwenye timu ya taifa kwa mara nyingine, namshukuru Kocha Mapeza na wengine wote,” alisema Kamusoko.


Kamusoko anakuwa mchezaji pekee wa Zimbabwe aliyecheza Ligi Kuu Bara msimu uliopita kuitwa katika kikosi cha nchi hiyo.

Baadhi ya wachezaji walioitwa na Mapeza ambao ni viungo ni Kamusoko, Devon Chafa (Caps United), Simon Shoko (FC Platinum), Kudakwashe Mahachi ( Golden Arrows), Khama Billiat (Mamelodi Sundowns), Marvelous Nakamba (Vittese), Danny Phiri (Golden Arrows), Liberty Chakoroma (Ngezi Platinum), Ovidy Karuru (AmaZulu) na Ronald Chitiyo wa Caps United.

No comments

Powered by Blogger.