Kilichompelekea IGP Mangu kutumbuliwa :Sirro Anena Haya Baada ya Uteuzi..!!!




Wakati mauaji ya watu zaidi ya 30 katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani yakiendelea kuumiza vichwa vya Watanzania, Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.


Kutenguliwa kwa uteuzi wa Mangu kutoka katika wadhifa huo kumetajwa kuwa huenda kumesababishwa na mfululizo wa matukio ya mauaji yaliyotokea katika wilaya hizo na miongoni mwa waliouawa wamo askari wanane waliokuwa katika doria.


Askari hao waliuawa katika Kijiji cha Jaribu mpakani mwa wilaya za Kibiti na Rufiji walipokuwa doria ya kukabiliana na matukio ya mauaji ya viongozi wa CCM, askari na raia baada ya gari lao kushambuliwa na wahalifu. Taarifa iliyotolewa jana jioni na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ilieleza kuwa Rais John Magufuli amemteua aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Mangu ambaye atapangiwa kazi nyingine.


Ingawa taarifa hiyo haikutaja sababu za kuondolewa kwa Mangu, wachambuzi wa masuala ya kijamii wanahusisha uamuzi huo na mauaji yaliyotokea katika wilaya hizo ambazo Serikali imeamua kuziundia kanda maalumu ya kipolisi ili kukabiliana na uhalifu.


Hadi sasa takriban watu 31 wameauawa katika wilaya hizo kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imezifuatilia kuanzia Mei, 2016.


Mauaji ya watu hao ambayo yameendelea kulaaniwa na watu mbalimbali, yamelifanya Jeshi la Polisi kupeleka kikosi maalumu kuimarisha usalama.


Pia, wakati wa uongozi wa Mangu yamewahi kuwapo matukio kadhaa ya uvamizi wa vituo vya polisi, askari kuuawa na kuporwa silaha.


Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alitembelea Kata ya Bungu wilayani Kibiti na kuzungumza na askari hao, sambamba na kuwataka wananchi kuwafichua wanaojihusisha na mauaji hayo. Mwigulu alisema Serikali haitaendelea kuvumilia kuona watu wakiuawa ilhali watuhumiwa wa mauaji wanafanya hivyo wakishirikiana na baadhi ya watu.


“Hakuna chama cha siasa ambacho kina thamani sawa na uhai wa binadamu, mtu kuwa chama anachotaka hajafanya kosa hata kustahili kuuawa, kwa maana hiyo mimi kila nikitafakari naona kuna kamchezo kanakochezwa, hatutawaacha wanaoua na wala hatutawaacha wanaoshirikiana na wanaoua,” alisema Mwigulu.


Sirro azungumzia uteuzi


Sirro ambaye aliteuliwa kushika wadhifa wa kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akitokea katika nafasi ya mkuu wa operesheni wa kanda hiyo, alisema kuwa anamshukuru Rais John Magufuli kwa kumwamini na kumkabidhi wadhifa huo ili awatumikie Watanzania. Alisema anamshukuru Rais kwa kumuona na kumuamini kwa utendaji wake wa kazi, hivyo hawezi kumuangusha.


“Tuombeane tu ndugu yangu hii nafasi si ndogo ni kubwa kwa Jeshi la Polisi, hivyo naomba ushirikiano kutoka kwenu na mengi nitaongea kesho (leo)” alisema Sirro.


Akizungumzia uteuzi huo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema uwajibikaji wa Sirro ndiyo chanzo cha kuteuliwa na Rais kwa nafasi hiyo. Alisema Sirro alikuwa mstari wa mbele kiutendaji.


Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete Desemba 30, 2013 alimteua Mangu akiwa Kamishna wa Polisi kuwa IGP akichukua nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Saidi Mwema aliyestaafu.


Kabla ya uteuzi wake huo ulioanza Januari Mosi, 2014 Mangu alikuwa Mkurugenzi wa Intelijensia ya Jinai katika Jeshi la Polisi.


Uvamizi wa vituo vya polisi


Baadhi ya matukio ya vituo vya polisi vilivyovamiwa na askari kuporwa silaha ni kama ifuatavyo; Julai 12, 2015 majambazi wenye silaha walivamia kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga na kuua askari wanne na raia watatu na kupora silaha.


Juni 12, 2014 katika kituo cha Polisi Mkamba Kimazichana majambazi wenye silaha walivamia kituo hicho na kuua askari polisi mmoja na mgambo na kupora silaha.


Juni 21, 2015 katika kituo cha Polisi Ikwiriri majambazi wenye silaha walivamia kituo hicho na kuua askari wawili na kupora silaha.


Januari 27, 2015 mjini Tanga, majambazi wenye silaha waliwajeruhi askari polisi wawili waliokuwa doria na pikipiki na kuwapora silaha.


Februari 3, 2015 wilayani Kilombero kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walivamia stoo ya kituo kidogo cha polisi Mgeta na kuiba silaha.


Machi 30, mwaka 2015 eneo la Kongowe Pwani, majambazi wenye silaha waliwaua askari wawili na kumjeruhi mmoja na kupora silaha.


Mei 29, 2015 jijini Dar es Salaam majambazi wenye silaha walivamia askari waliokuwa lindo eneo la Tazara na kupora silaha.


Aprili 13, 2017 askari polisi waliokuwa wakirejea katika kambi yao iliyopo Bungu wilayani Kibiti walishambuliwa kwa risasi na majambazi. Katika tukio hilo askari wanane waliuawa na silaha ziliporwa.


Februari 21, 2017 ofisa upelelezi wa polisi wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya, mlinzi wa kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu Shabani Ngamba na Peter Katundu aliyekuwa akikusanya ushuru wa Serikali wa Halmashauri ya wilaya ya Kibiti, waliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliovamia kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu katika kijiji cha Jaribu kata ya Mjawa wilayani Kibiti.

No comments

Powered by Blogger.