Maduro aitisha bunge la katiba
Rais wa Bunge la Venezuela ametoa wito kwa raia wa nchi huyo kuiasi serikali na kutokubali kile alichokiita "mapinduzi" yanayotaka kufanywa na Rais Nicolas Maduro, ambaye ametangaza kuitishwa kwa bunge la katiba.
Julio Borges amesema hatua ya Maduro kuitisha bunge la katiba ni "udanganyifu mkubwa" unaofanywa na kiongozi huyo na wasaidizi wake ambao una lengo la kuwabakisha madarakani.
Borges ameongeza kuwa hatua hiyo itawanyima raia wa Venezuela haki yao ya kuelezea maoni yao kupitia kura, na badala yake amelitaka jeshi kuzuia kutokea kwa "mapinduzi" hayo ya Maduro.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Caracas hapo jana, Borges alisema: "Wanachokitaka watu wa Venezuela sio kubadilisha katiba bali kumbadilisha Maduro kupitia kura."
Kauli ya Julio Borges inakuja chini ya masaa 24 tangu Rais Maduro kutoa amri ya kirais ambayo inaruhusu kufanyiwa marekebisho kwa ofisi za umma, akisema kuwa ni muhimu kupambana na kile alichokiita "mapinduzi ya kifashisti", anayodai yanaongozwa na Marekani.
Akizungumza kwenye sherehe za Mei Mosi mjini Caracas hapo jana, Maduro alisema ni lazima sasa nchi yake isonge mbele kutoka wimbi la machafuko na maandamano makubwa yaliyosambaa sehemu mbalimbali za taifa hilo la Amerika ya Kusini.
"Katika siku hii ya kihistoria, Mei Mosi, nitasaini notisi ya kutumia nguvu za kikatiba kuitisha bunge la katiba la wananchi mara moja kuandaa mkutano wa katiba ya watu, litakalochaguliwa kidemokrasia na moja kwa moja kutoka kwa watu wenyewe," alisema Maduro.
Maandamano yapamba moto
Waandamanaji wanazidi kumiminika kwenye mji mkuu wa Venezuela, Caracas, wakimtaka Rais Nicolas Maduro ajiuzulu.
Hatua hii ya Maduro inaakisi ya mtangulizi wake, Marehemu Hugo Chavez, ambaye mwaka 1999 aliitisha Bunge la Katiba lenye wajumbe 131 kutoka makundi mbalimbali na kuandika katiba ya sasa ya Venezuela. Rasimu ya katiba hiyo ilipitishwa kwa kauli moja kwenye bunge hilo.
Lakini wakati huo, kiongozi huyo mwenye mvuto alikuwa bado anaungwa mkono na umma, kinyume na Maduro ambaye uchunguzi wa maoni unaonesha anapigwa na Wavenezuela saba katika kila kumi.
Haya yanatokea huku maandamano makubwa ya kumpinga Rais Maduro yakiendelea kwenye mji mkuu, Caracas.
Venezuela imekuwa na maandamano ya kila siku, tangu Mahakama ya Juu ilipojaribu kulipunguzia madaraka bunge ambalo linatawaliwa na wapinzani mapema mwaka huu.
Kiongozi wa upinzani, Henrique Capriles, anasema hatua ya Maduro kuitisha bunge la katiba ni njia ya kujibakisha madarakani kinyume na katiba, na akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter hivi leo, ametowa wito kwa wananchi kuiziba mitaa yote ya mji mkuu, Caracas, kwa maandamano makubwa ya umma.
"Watu, miminikeni mitaani. Lazima muuasi upuuzi kama huu!" ameandika Capriles, ambaye mwaka 2013 alishindwa kwa kura chache na Maduro katika uchaguzi mkuu
Post a Comment