Misri yalipiza kisasi mauaji ya wakristo 28
Wanajeshi wa Misri wametekeleza mashambulizi ya angani katika taifa jirani la Lybia ambapo wamelenga kambi za mazoezi za wapiganaji wa kijihadi.
Maamlaka zinasema mashambulizi hayo karibu na mji wa mashariki wa Derna ni ya kulipiza kisasi shambulizi la hapo jana katikati mwa Misri.
Watu 28 waliuwawa baada baada ya washambuliaji waliojifunika nyuso kuvamia basi lililokuwa limebeba wakristo wa dhehebu la Coptic.
Misri ilianza mashambulizi ya kulipiza kisasi saa chache tu baada ya mauaji hayo, hata kabla ya kundi lolote kutoa madai ya kuhusika na shambulizi hilo.
Vyanzo vya idara ya jeshi vinaarifu kwamba wanaanga wa Misri walitekeleza mashambulizi sita katika kambi iliyo karibu na mji wa Derna mashariki ya Lybia.
Maamlaka zinasema zilidhibitisha kwamba washukiwa wa shambulizi la jana walipokea mafunzo ya kivita katika kambi hiyo.
Sio mara ya kwanza ambapo misri imetekeleza mashambulizi sawa na hayo nchini Lybia karibu na mpaka wake wa magharibi.
Mwaka 2015, Misri ilitekeleza mashambulizi ya angani baada ya kundi la kigaidi la Islamic state kutoa kanda ya video ikionyesha mauaji ya wakristo 21 wa dhehebu la coptic.
Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi anasema Misri itawalinda raia wake vilivyo, na itashambulia mahali popote pale.
Post a Comment