MUGABE AMTEUA BINTI YAKE VITENGO NYETI KWA MARA YA PILI NDANI YA WIKI MOJA

BINTI wa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ameteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya benki mpya nchini humo, ikiwa ni mara ya pili kupata uteuzi ndani ya wiki moja.

Bona (27) mapema wiki hii aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Sensa, jambo ambalo lilisababisha ‘mashambulizi’ dhidi ya Rais kuwa amempendelea na anataka kuiweka familia yake katika nafasi nyeti.

Wakati habari hizo zikiwa bado za motomoto, gazeti la Independent la nchi hiyo limesema binti huyo ameteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Benki ya Empower, ambayo inamilikiwa na serikali kwa aisilimia 100.

Kuibuliwa kwa taarifa hizo kumesababisha mitandao ya kijamii kushadadia na kusema Bona anaandaliwa mazingira ya kupewa nafasi za juu serikalini wakati ‘umri wa baba yake ukienda saa za magharibi’. Mugabe kwa sasa ana umri wa miaka 93.

Gazeti hilo lilimkariri Waziri anayeshughulikia masuala ya uzawa, Patrick Zhuwao, ambaye ni mpwa wa Mugabe kuwa Bona na maofisa wengine wawili vijana wameteuliwa kuwa wajumbe wa bodi hiyo si kwa sababu ya taaluma zao bali kutokana na sera ya wizara kuwapa nafasi vijana.

Pamoja na kulalamikiwa kuwa anapendelewa kutokana na kuwa mtoto wa Rais, Bona ana sifa ya kuwa mjumbe wa bodi hiyo kwa kuwa ana shahada ya uzamili katika masuala ya benki na fedha kutoka Singapore.Hata hivyo, hakuna rekodi zinazoonyesha kuwa alishawahi kufanya kazi benki baada ya kuhitimu elimu yake ya chuo kikuu.

Licha ya kwamba Mugabe hajamtaja mrithi wake pamoja na umri wake kuwa mkubwa, kumekuwa na minong’ono kwamba kiongozi huyo, baba wa watoto watatu, anataka kuweka mazingira kuhakikisha familia yake inaendelea kubaki katika maeneo ya fedha na siasa baada ya kufariki dunia.

No comments

Powered by Blogger.