SHAHIDI WA GWAJIMA NI KIBOKO YAO!!!! TAZAMA HAPA JINSI ALIVYOWAFANYA POLISI MAHAKAMANI ILI KUMCHOMOA GWAJIMA KATIKA KESI YA SILAHA
MUUGUZI wa Hospitali ya TMJ, Devotha Bayona, amedai mahakamani katika kesi ya kushindwa kuhifadhi silaha inayomkabili Askofu Mkuu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (47), askari polisi walichukua sanduku lililokuwa na silaha kwa nguvu kutoka kwake.
Kadhalika, Bayona amedai kuwa sanduku hilo lilikuwa wodini pembeni ya kitanda alichokuwa amelazwa Askofu Gwajima na kwamba mshtakiwa huyo alikataa kulitoa, lakini baada ya kusikia mvutano alimwagiza muuguzi kulitoa na kuwakabidhi askari hao.
Ushahidi huo ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala.
Alidai kuwa Machi 29, 2015 aliingia kazini zamu ya usiku kuanzia saa 2:00 hadi saa 2:00 asubuhi.
Alidai kuwa baada ya kuingia kazini eneo lake la kazi lilikuwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), na mara alisikia mlango unagongwa. Alipofungua, aliendelea kudai, aliwakuta watu watatu, wawili walijitambulisha kwamba ni askari polisi na mwingine ni msaidizi wa Askofu Gwajima.
"Nilipofungua mlango niliona watu watatu, walipojitambulisha, nilirejea ndani kumhoji mgonjwa kuhusu ujio wa askari na msaidizi wake, alikiri kweli Yekonia Bihagaze ni msaidizi wake," alidai shahidi huyo na kueleza zaidi:
"Askari polisi waliniambia wanahitaji sanduku la mgonjwa lililokuwa kando ya kitanda chake pale wodini... nilimjulisha askofu (lakini) alikataa nisitoe sanduku lake kwa sababu lilikuwa na bastola yake ndani."
Akifafanua zaidi, shahidi alidai kuwa aliwajulisha wale askari pamoja na msaidizi wa askofu kwamba utaratibu wa kuchukua hilo sanduku wanatakiwa kuandika maelezo ya kuchukua mali hiyo kutoka kwa mgonjwa.
Hata hivyo, askari walimjibu kwamba watapeleka maelezo hayo kesho yake.
"Askofu aliniita akanieleza amesikia mvutano kuhusu hilo sanduku nichukue nimpe msaidizi wake awakabidhi askari," alisema Bayona.
"Nilifanya kama mgonjwa alivyoniagiza, niliwakabidhi askari baada ya kung'ang'ania kutaka kuingia kwa nguvu wodini kuchukua sanduku hilo."
Alidai baada ya kukabidhi hakujua kilichoendelea kwa sababu alianza kumhudumia mgonjwa ambaye alipata msongo wa mawazo (stress) kutokana na tukio lile kubwa.
Mbali na Askofu Gwajimba na Bihagaze, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Mzava na Georgey Milulu. Wote wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa wakimiliki bastola aina ya Berretta pamoja na risasi 20 kinyume cha sheria.
Wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A walikutwa wakimiliki bastola aina ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Iliendelea kudaiwa kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1) na cha 34 (1)(2) na(3) cha sheria ya silaha na milipuko sura ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Pia, inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao pia walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola na risasi 17 za bunduki aina ya shotgun.
Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo juzi, mshtakiwa wa nne na mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Milulu alidai hakuwa anajua kama Askofu Gwajima anamiliki bastola hadi siku aliposikia ushahidi wa Jamhuri dhidi yake.
Aidha, Mzava pia juzi aliieleza mahakama kuwa hajawahi kukutwa na begi lolote katika hospitali ya TMJ kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka na kwamba bastola na risasi anavyoshitakiwa navyo aliviona kwa mara ya kwanza mahakamani
Post a Comment