Ray kigosi atoa povu kwa uongozi wa Yanga.....
Kwa siku za karibuni Wekundu wa Msimbazi wamekuwa gumzo sana mtaani kutokana na fujo wanazoendelea kuzifanya katika dirisha la usajili, hadi sasa Simba wameshanunua majina makubwa kama Aishi Manula, Shomari Kapombe huku John Raphael Boko naye akitajwa kuhamia katika klabu hiyo.
Wakati Simba wanafanya hivyo, huko Chamanzi nako matajiri wa Azam wananunua tu wachezaji na hadi sasa wamewazidi Yanga kwa kuchukua wachezaji watatu ambao Yanga nao walikuwa wanawataka ambao ni Mbaraka Yussuf, Wazir Juniour na Salmini Hoza kutoka Mbao FC.
Wakati Simba na Azam wakifanya hivyo, kwa upande wa mabingwa wa Tanzania klabu ya Yanga hali imekuwa tofauti sana na ilivyozoeleka kwani hakuna taarifa yoyote ya usajili iliyotolewa ndani ya klabu hiyo huku wakisema mambo yao safari hii ni kimya kimya hawataki kelele.
Ukimya huu umekuwa ukiwaumiza sana mashabiki wa klabu hiyo haswa kutokana na usajili unaofanywa na wapinzani wao. Moja kati ya mashabiki wakubwa wa Yanga ni muigiza filamu wa Tanzania Vicent Kigosi almaaru kama Ray ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram ameamua kufunguka anavyojisikia kuhusu ukimya wa klabu yake hiyo.
“FREEDOM OF SPEECH;Viongozi wangu muliopo madarakani katika uongozi wa Yanga kwa sasa munachotakiwa kujua ni kwamba tunaoumia sana ni sisi wanachama na mashabiki, hali ya ukimya na sintofahamu wa uongozi wetu haswa katika kipindi hiki cha usajili inatia mashaka” alianza kwa kuandika hivyo.
“Ni wazi kuwa kwa sasa timu imewashinda na sio siri tena kwamba Yanga hatuna pesa ya kusajili na hata ya kuwabakiswha waliopo na ni muda muafaka sasa wa kumkodisha Manji timu ili iwe “Yanga yetu” na hilo ni bora kuliko kudhalilika na nashauri tufanye maamuzi ya haraka na mtu akitokea kupinga tumpe yeye timu”
Ray aliendelea kusisitiza “hakuna kipindi mashabiki wanakuwa na furaha kama kipindi hiki cha usajili na hali ni tofauti kwa sisi mabingwa mara 3 wa Tanzania, hakuna tunachohitaji sisi mashabiki zaidi ya furaha na furaha huletwa na ushindi na ushindi huletwa na wachezaji bora na wachezaji bora husajiliwa kwa pesa nyingi na chini ya Manji tulitembea kifua mbele leo ameondoka hata nusu mwaka haujafika tumeanza kuwa chini”
Ray aliwasisitiza viongozi kuitisha mkutano mkuu haraka huku akiwaambia kwamba Manji ana mahaba na klabu hiyo na wao kama mashabiki watapiga kelele kumuomba hadi akubali kuichukua timu hiyo huku akikiri kwamba tangu akiwa mtoto hajawahi kuona mambo makubwa kama yaliyofanywa na Yusuph Manji.
Post a Comment