Ikulu Yajibu Acacia Kuhusu Mchanga wa Madini
Uamuzi wa serikali kuhusu suala la kusafirisha mchanga wa madini kwenda nje ya nchi utategemea ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa na Rais Magufuli kuchunguza sakata hilo.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa ikiwa ni siku moja tangu Kampuni ya Acacia ilipotaka kuundwa kwa kamati huru ya kuchunguza kiasi cha madini kilichomo kwenye makinikia hayo.
“Sijui chochote kuhusu hao Acacia kuomba iundwe kamati huru , lakini tunasubiri ripoti ya kamati ya pili iliyoundwa kuchunguza sakata hili wampelekee ripoti Rais,” alisema Msigwa.
Kamati ya awali iliyokuwa ikiongozwa na Prof. Mruma ambayo ilikabidhi ripoti yake Mei 24 mwaka huu ilionyesha kuwa kiwango cha madini yaliyomo kwenye makinikia hayo ni zaidi ya yale ambayo hujazwa kwenye makabrasha.
Mbali na kuonekana kiasi kuzidi, lakini kamati hiyo ilibaini pia kuna madini makakati (strategic metals) ambayo yamo kwenye makinikia hayo lakini hayakuwa yakitajwa na kampuni zinazosafirisha mchanga nje jambo lililosababisha serikali kupata hasara ya mabilioni.
Kwa upande wao Acacia, walipinga ripoti hiyo na kusema wao hutangaza kila kitu kwa mujibu wa sheria na kulipa tozo zote stahiki hivyo kuomba iundwe kamati huru kuchunguza upya kiasi cha madini kwenye mchanga huo.
Post a Comment